Furaha ndio kitu pekee ambacho hutafutwa kwa gharama kubwa na kila mtu, awe tajiri ama maskini.
Kosa kubwa ambalo watu wengi kufanya ni kushindwa kutambua ni wapi ambapo kitengo cha furaha hupatikana. Wengi hufikiri kwamba labda baada ya kutafuta kitu fulani na kukipata ndipo watapata furaha, lakini cha kushangaza ni kwamba hakuna kitu ambacho wanaambulia.
Na kosa kubwa ni kwamba, wengi hatujui ni nini hasa kinachosababisha furaha, ni kitengo kipi ambacho husababisha furaha.
Sasa ili kuhakikisha kwamba nataka uelewe, ni kipi hasa ni kitengo cha furaha, nimekuandalia dhana ya kula chakula na jinsi mfumo unavofanya kazi. Hamna namna usipofuata mfumo ambao ndio kanuni huwezi kufikia malengo yako kwa sababu ni kama unatoka nje ya mstari.
Wakati wa kula chakula, huwa kuna vitengo vitatu ambavyo mtu hushiriki katika utamu wa kula chakula. Simaanishi kwamba anakula sehemu tatu bali namaanisha kwamba, chakula cha aina moja anashiriki kula mara tatu.
Watu wengi huwa tunafikiri kwamba ni ulimi pakee ndio huonyesha ladha ya chakula, na tunasahau maeneno mawili ambayo humlidhisha mtu wakati wa kula chakula.
Eneo la kwanza ni kula chakula bila kukiona, ama kukitia mdomoni. Hapa mtu anaweza kufurahia harufu peke yake bila hata kugusa chakula na kutia mdomoni. Hakuna harufu nzuri ya chakula kama harufu ya chakula ambacho hukili, yaani unatamania tu. Kwa harufu na kuhisi bila kushiriki kimwili mtu anaweza kujiburudisha. Eneo hili ili ulidhike vizuri ni lazima uwe na shukrani kubwa sana.
Eneo la pili ni kinywani, hiki ni kitengo ambacho kila mtu anakifahamu kwa sababu hapa kila mtu huwa anajiona kila kitu anachofanya. Ladha ya chakula hapa kila mtu anaitambua kwa ulimi, kuonja. Eneo hili unaweza kula chakula na kufurahia bila wasi, haijarishi ni kingi ama kidogo. Mwenye shukrani atafurahia.
Eneo la tatu ni tumboni. Sasa eneo hili halina tabu kwa sababu ndio mwisho wa chakula. Hili ni eneo ambalo chakula kinajaa tumboni, tumbo linakuwa limejaa lakini huwezi kuhisi harufu wala utamu bali kwenye tumbo usawa wa ujazo tu pekee. Kiasi kinaongoza. Mwenye shukrani atafurahia.
Leo napenda niongelee eneo la pili, eneo mchakato, eneo ambalo lazima kinywa kicheze. Ili uone ladha ya chakula kwa ulimi lazima uvunjevunje kile unakula. Ndipo ulimi wako utaona ladha ya chakula unachokula.
Na katika maisha ndivyo mambo yalivyo lazima uvunjevunje kile unafanya. Kama hutovunjavunja huwezi kuona chochote. Angalia jinsi kinywa chako kilivo, ulimi ni laini na hauna mifupa, meno ni magumu. Na kinachofanya chakula kiwe kitamu ni ushirikiano kati ya sehemu ngumu na laini.
Magumu yote unayopitia ndio ladha ya maisha. Utamu unakuwepo pale chakula kinamegwa megwa. Chakula kikifika tumboni hakina ladha na ndio maisha jinsi yalivyo, ukifikia ukamirifu huwezi kufurahia maisha. Na ndio maana Mungu alificha hekima, ili watu wawe wanatia juhudi katika kuifichua na kwa sababu inapatikana kwa gharama kabla haijafichuka na ikifichuka inakuwa na gharama kubwa kwa wasioijua kwani kwao ni giza tu.
Furaha kubwa katika maisha ni kugundua jambo jipya, (harufu), nguvu ya kuishi katika maisha ni kuliendea jambo jipya, (mchakato kinywani). Ushindi mkubwa katika maisha ni kufichua jambo jipya.( tumboni). Hizi ndizo zana tatu katika maisha, unazoweza kuishi kwa kutumia mfumo wa chakula.
Jambo moja ambalo unapaswa kujua ni kwamba, ushindi haupagi mtu furaha, bali mashindano ndiyo humpa mtu furaha. Kusinzia ni kutamu kuliko kulala. Ukifikia Mafanikio utakuwa unatamani kupata kingine kwahiyo kama unategemea matokeo ya jambo huwezi kufurahia maisha. Linda sana eneo la harufu na ladha. Harufu inakupa matumaini mapya, ladha inakupa nguvu ya kuyaendea matumaini.
Angalia kinywa chako kina meno ambayo ni magumu, na ulimi ambao ni laini. Bila ushirikiano wa vitu hivyo viwili chakula hakina ladha.
Usiogope mapito uliyopitia, usiangalie mabaya pekee bali angalia na mazuti uliyonayo. Hata kama wewe ni nani, tafuta jambo la kufanya, lifanye kwa moyo na hekima ya kujifunza kutoka katika mapito yako.
Ukipitia maisha magumu hapo nyuma, kupambambanua hekima ni rahisi kwa sasa kwa sababu tayari ulikuwa ndani ya mchezo. Ukipitia maisha laini, kupambanua maisha sasa inahitaji kutia juhudi kwa sababu huna mapito. Kwa hiyo mapito ni zawadi kwa wenye shukrani ili kuishi maisha ya furaha.
Ukawe na tafakari njema.
Sadick Kilasi wa jikolaushauri.blogspot.com.
Mawasiliano ni 0687000768 au sadikila65@gmail.com.
0 comments:
Post a Comment