Kuna wakati ambao huwa tunahisi kukosewa sana na wale watu wa karibu yetu, na hivyo akili zetu haraka kabisa hutufanya tuone wale wengine hawastahili na sisi ndio tubastahili. Kwa maana hiyo huwa tunawafunga hao watu gerezani, na gereza ambalo huwa tunawafunga ni katika Ubongo wetu. Baada ya kuwafunga shughuli inayofuata huwa ni ulinzi. Ubongo wetu huwa unang'ang'ania kwamba lazima mfungwa wetu tusimwachilie kirahisi lazima aonekane mwovu na lazima tumchunge ili asitoke kabisa.
Bila kujua kwamba tunajiumiza wenyewe kwa kung'ang'ania kuwaona wengine hawastahili. Haina maana kwamba mtu akikosea asiambiwe lakini kuna njia namna ya kumwambia mtu. Na njia hii itatusaidia sisi tusimtie mtu gerezani.
Njia yenyewe ni; mtu akikukosea mwonye lakini kumbuka na wewe wale uliowakosea, kwa kufanya hivi unajaribu kuona mwingine hastahili na wewe pia hustahili na mwisho mnatengeneza usawa.
Paulo anasema, Wagalatia 6:1-5, Ndugu zangu, mtu akighafirika katika kosa lolote, ninyi mlio wa Roho mrejezeni upya mtu kama huyo kwa roho ya upole, ukijiangalia nafsi yako usije ukajaribiwa wewe mwenyewe. Mchukuliane mizigo na kuitimiza hivyo sheria ya Kristo. Maana mtu akijiona kuwa ni kitu, naye si kitu, ajidanganya nafsi yake. Lakini kila mtu na aipime kazi yake yeye mwenyewe, ndipo atakapokuwa na sababu ya kujisifu ndani ya nafsi yake tu, wala si kwa mwenzake. Maana kila mtu atalichukua furushi lake mwenyewe.
Kila mtu aliyepo duniani ni mdhamini wa makosa yake na ndiomaana tunajitaidi kuonyesha kwamba sisi si watenda makosa wakati wote.
Anza kuwa na huruma badala ya kuhukumu.
Kujiweka nafasi ya wengine ni moja ya mlango wa utumishi wa kikuhani, na kila mmoja aliyezaliwa upya huyo ni kuhani wa Kristo.
Ufunuo Wa Yohana 5:10, ukawafanya kuwa ufalme wa makuhani kwa Mungu wetu; nao qanamiliki juu ya nchi.
Mambo Ya Walawi 16:21, Na Haruni ataweka mikono yake miwili juu ya kichwa cha yule mbuzi aliye hai, na kuungama uovu wote wa wana wa Israeli, makosa yao, naam, dhambi zao zote; ataziweka juu ya kichwa chake, kisha atampeleka aende jangwani kwa mkono wa mtu aliye tayari.
Kuhani alikuwa anawakilisha jumuiya yote ya wana wa Israeli ili kumtwisha dhambi mbuzi na dhambi za watu zilitakasika kupitia tendo moja la kuhani wao.
Ikiwa tupo tayari kujiweka nafasi ya wengine na kuwaombea wale wanatukusea na kuwapenda zaidi hapo tunaonyesha tendo la ukomavu wa kiroho.
1Petro 2:5, Ninyi nanyi, kama mawe yaliyo hai, mmejengwa mwe nyumba ya Roho, ukuhani mtakatifu, mtoe dhabihu za roho, zinazokubaliwa na Mungu, kwa njia ya Yesu Kristo.
Kuwa tayari kujiweka nafasi ya wengine ili uingie patakatifu pa BWANA. Kujiweka nafasi ya wengine ni moja ya milango ya kuingia patakatifu.
Sasa, anza kujiweka nafasi ya wengine na waombee wanaokukosea, waweke watu hao mbele za Mungu.
Ukiwa tayari leo, kuwaombea hao kwa Mungu, na kuteseka kwaajili yao kwa muda mwingi ukiwaombea, hakika utaona utofauti.
Waefeso 6:18, kwa sala zote na maombi mkisali kila wakati katika Roho, mkikesha kwa jambo hilo na kudumu katika kuwaombea watakatifu wote.
Asante.
Sadick Kilasi wa jikolaushauri.blogspot.com.
Mawasiliano ni 0687000768 au sadikila65@gmail.com.
0 comments:
Post a Comment